MESSI HATARINI KUTOCHEZA KOMBE LA DUNIA 2018
Argentina, na mshambuliaji wao nyota Lionel Messi, wamo hatarini ya kukosa kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1970 baada ya kutoka sare tasa na Peru.
Ni nchi nne pekee za Amerika Kusini ambazo zinahakikishiwa nafasi katika michuano hiyo itakayofanyika Urusi mwaka 2018.
Argentina wamo katika nafasi ya sita wakiwa wamesalia na mechi moja pekee.
Mabingwa hao wa dunia mara mbili ni lazima washinde mechi yao ya mwisho ya kufuzu dhidi ya Ecuador kuwawezesha kufika angalau nafasi ya tano ambayo itawapatia fursa ya kucheza mechi mbili za muondoano za kufuzu dhidi ya New Zealand.
Mechi za mwisho zitachezwa saa nane usiku Afrika Mashariki Jumatano mnamo 11 Oktoba.
Mkufunzi wa Argentina Jorge Sampaoli amekiri kwamba mambo zi mazuri lakini akaongeza kwamba ana imani kuwa iwapo timu hiyo itacheza ilivyocheza dhidi ya Peru, basi watafuzu kwa Kombe la Dunia.
Lionel Messi aligonga mlingoti wa goli kipindi cha pili.
Sampaoli amesifu bidii ya mchezaji huyo wa Barcelona ambaye aliunda nafasi nyingi sana za kufunga ingawa wenzake walishindwa kufunga.
Mechi hiyo ilichezewa uwanja wa La Bombonera unaotoshea mashabiki 49,000 mjini Buenos Aries.
Argentina, ambao walimaliza wa pili Kombe la Dunia 2014, wanatoshana kwa alama na Peru walio nafasi ya tano, alama 25.
Tofauti yao ya mabao ni sawa pia (+5).
Peru hata hivyo wako mbele kwa sababu wamefunga mabao mengi.
Ushindani ni mkali sana kundini kwani ni alama nne pekee zinaotenganisha Uruguay walio wa pili (28) na Paraguay (24) walio nafasi ya saba.
Ushindi kwa Argentina unaweza hata kutosha kuwawezesha kufuzu moja kwa moja.
Hata hivyo, Argentina wametoka sare mechi zao tatu za kufuzu walizocheza hivi karibuni zaidi.
Aidha, rekodi yao katika mji mkuu wa Quito nchini Ecuador, mji ulio mita 2,900 juu ya usawa wa bahari ni duni mno.
Wameshindwa mechi mbili kati ya tatu walizocheza karibuni zaidi uwanjani humo, hiyo ya tatu ikiwa sare.
Ecuador hata hivyo nao wameshindwa mechi zao tano za karibuni zaidi za kufuzu Kombe la Dunia.
Peru watakuwa wenyeji wa Colombia na iwapo watatoka sare, Argentina watapoteza nafasi iwapo hawatashinda mechi yao.
Chile, walio nafasi ya tatu watacheza dhidi ya Brazil ambao tayari wamefuzu, huku nao Uruguay, ambao wanakaribia sana kujihakikishia nafasi ya michuano hiyo ya Urusi kwa sababu ya wingi wa mabao yao, wanahitaji sare pekee dhidi ya Bolivia ambao tayari wameondolewa, ili kufuzu.