Azam Fc Kufuatwa na Simba na Yanga Chamazi
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa ratiba mpya ya Ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuifanyia marekebisho ratiba ya awali, ambapo mechi kati ya Azam FC na Simba SC imepangwa kupigwa Jumamosi ya Septemba 9, katika dimba la Azam Complex Chamazi, saa 1:00 usiku.
Mabadiliko hayo yameigusa Azam kwa kiasi kikubwa ambapo sasa mechi zake zote za nyumbani zitakuwa ni saa 1:00 usiku na itatumia uwanja wa Chamazi ukiwemo mchezo dhidi ya Yanga utakaopigwa Desemba 29, mwaka huu, na itakuwa ni mara ya kwanza kwa vilabu vya Simba kucheza na Azam FC katika dimba la hilo lililopo Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Katika ratiba hiyo mpya ya ligi, mechi ya watani wa jadi katika soka la Tanzania Yanga dhidi ya Simba imepangwa kupigwa Oktoba 28, 2017 huku mchezo wa marudio ukiwekwa kiporo raundi ya 23, Machi 14 mwakani, kutegemeana na safari ya timu hizo katika michuano ya Afrika.
Marekebisho hayo yamefanywa na kikosi kazi cha watu wanne kilichopewa kazi maalum ya kuipitia upya ratiba ya awali kwa agizo la rais wa TFF, Wallace Karia baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau kufuatia michezo ya raundi ya pili ya ligi msimu huu kuahirishwa ili kupisha kalenda ya FIFA.
Ratiba hiyo ya sasa imezingatia michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA, michezo ya kimataifa kwa vilabu vya Simba na Yanga, pamoja na mechi za kombe la shirikisho la Azam Sports.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo mpya, mechi nyingine zitakazopigwa Septemba 9, saa 10 jioni itazikutanisha Tanzania Prisons Vs Majimaji katika dimba la Sokoine Mbeya.
Jumapili ya Septemba 10, zitapigwa mechi sita kama ifuatavyo:-
Njombe Mji Vs Yanga
Mtibwa Sugar Vs Mwadui FC
Lipuli Vs Stand United;
Singida United Vs Mbao;
Kagera Sugar Vs Ruvu Shooting
Mbeya City Vs Ndanda FC
Baada ya mzunguko huo wa pili, mzunguko wa tatu wa ligi hiyo utaendelea tena Septemba 15, 16 na 17 kwa timu zote 16 kukiwasha kama ifuatavyo.
Septemba 15 ni Azam Fc Vs Kagera Sugar katika dimba la Chamazi, mchezo ukipigwa saa 1:00 usiku.
Septemba 16 ni:
Majimaji FC Vs Yanga SC
Mtibwa Sugar Vs Mbao FC
Prisons Vs Ndanda FC
Lipuli Vs Ruvu Shooting
Stand United Vs Singida United
Septemba 17 kutakuwa na mechi mbili ambazo ni Mbeya City dhidi ya Njombe Mji dimba la Sokoine Mbeya, huku Simba ikiikaribisha Mwadui FC katika dimba la Uhuru.