TAARIFA ZA AWALI KUHUSU KULIPULIWA KWA OFISI YA IMMA ADVOCATES ZATOLEWA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam mnamo tarehe 26/8/2017 lilitoa taarifa ya awali ya tukio la mlipuko uliotokea katika ofisi za mawakili wa IMMMA zilizopo katika eneo la Upanga jijini Dar Es Salaam.
Hivyo Jeshi la Polisi linapenda kuufahamisha umma kuwa uchunguzi wa awali uliofanyika umebaini kwamba usiku wa kuamkia tarehe 26/8/2017 majira kati ya saa 7:00-8:00 watu wasiojulikana utambulisho wao na idadi kamili, walifika katika ofisi za mawakili wa kampuni ya IMMMA (IMMMA ADVOCATES) wakiwa na magari mawili wakijifanya ni askari na kuwarubuni kisha kuwachukua walinzi wa jengo hilo na kuondoka nao kwenye moja ya gari walilokwenda nalo, ambapo baadaye walinzi hao walikutwa maeneo ya Kawe wakiwa hawajitambui.
Aidha, kundi lililobaki liliingia ndani ya Ofisi hizo na kuweka milipuko iliyotengenezwa kienyeji ambayo baada ya watu hao kuondoka ililipuka na kusababisha uhalibifu wa mali na jengo la ofisi hiyo pamoja na majengo ya jirani.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu hao waliofanya tukio hilo pamoja na kujua dhamira yao ili wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.
Aidha tunapenda ifahamike kuwa wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda maisha ya watu na mali zao hivyo kamwe haliwezi kutumika kuhujumu maisha ya watu na mali za wananchi.
Tunaomba waathirika wa tukio hili na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi wa tukio. Vilevile, tunatoa rai kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia katika upelelezi waziwasilishe kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi.
B.M. KITALIKA- SACP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM