MKOA WA LINDI KUWA MWENYEJI KATIKA MAONESHO YA NANE NANE KITAIFA
Maonesho ya Kilimo (NaneNane) Ambayo yameanza Agosti 1, 2017 kote nchini kwa ngazi mbalimbali za kanda huku Maonesho hayo Kitaifa yakifanyika Mkoani Lindi huku Maandalizi na maonesho ya Ki-Kanda yanaratibiwa na uongozi wa mikoa husika.
Maandalizi ya Maonesho ya 24 ya kilimo na sherehe za Nanenane yatafanyika kwa siku 8 ambapo Kitaifa yatafika ukomo jioni ya Agosti 8, 2017 katika Viwanja vya Ngongo na Maeneo mengine yatakapoadhimishwa kikanda katika viwanja vya maonesho ni John Mwakangale –Mbeya; Mwalimu J.K. Nyerere –Morogoro; Themi – Arusha; Nzuguni - Dodoma; Nyahongolo – Mwanza; na Fatuma Mwassa - Tabora.
Maonesho ya mifugo sanjari na Maonesho ya Kilimo hutoa changamoto ya kuleta mapinduzi katika Ufugaji, Uvuvi, na Kilimo na kutoa ajira hususani kwa vijana kuwaongezea zaidi kipato na kuondoa umasikini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg Mathew Mtigumwe wakati akizungumza na kueleza muktadha wa Maonesho hayo ambayo Kitaifa yanafanyika Mkoani Lindi na kubebwa na kauli mbiu mahususi kwa mwaka huu 2017 isemayo "Zalisha kwa Tija Mazao ya Bidhaa za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati"
Malengo ya maonesho hayo ni utoaji elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, mashirika ya umma na binafsi.
Teknolojia/Bidhaa zitakazooneshwa ni pamoja na zana za Kilimo, Mbegu bora za mazao mbalimbali, Uzalishaji wa mazao katika mazingira yaliyodhibitiwa ambapo piaTaasisi za kitafiti ambazo zitaonyesha teknolojia mbalimbali za kuongeza tija zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali, Utengenezaji wa chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, Uboreshaji wa viasilu ili kupata mifugo na mazao ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa kutokana na maeneo walipo wananchi wanaohitaji kujihusisha na ufugaji na kilimo na udhibiti wa magonjwa.
Pia uzalishaji bora wa mazao ya nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa mayai, Kuongeza thamani mazao ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, ambapo Taasisi za elimu zitaonyesha ubunifu wa kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji wakubwa na wadogo wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.
Maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane yohusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi, mabenki, Taasisi za umma na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali