MATOKEO YA AWALI YA UCHAGUZI NCHINI KENYA YADAI UHURU KENYATTA ANAONGOZA

Kura zinaendelea kuhesabiwa na matokeo kutangazwa baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Jumanne. Katika matokeo yaliyokuwa yametangazwa kufikia saa tatu asubuhi Jumatano, Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alikuwa akiongoza akiwa na kura 7,461,933 (54.64%) akifuatwa na Raila Odinga wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) aliyekuwa na kura 6,079,136 (44.51%). Matokeo hayo ni ya vituo 36659 kati ya 40,883. Kura ambazo zilikuwa zimeharibika kufikia wakati huo ni 353,389. Muungano wa Nasa umepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa na tume hiyo na kusema si sahihi. Bw Odinga amesema IEBC imefanya makosa kwa kutangaza matokeo hayo bila kuwaonyesha maajenti wa vyama Fomu 34A, kubainisha matokeo hayo yametoka katika vituo gani. Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo. Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki. Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa. Wengi wanahofia uwezekano wa kutokea tena kwa ghasia za baada ya uchaguzi sawa na ilivyotokewa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Watu zaidi ya 1,100 walifariki na wengine 600,000 kuachwa bila makao. Tume ya uchaguzi imetangaza matokeo kutoka kwa vituo 36659 kati ya jumla ya vituo 40883 ambapo: Uhuru Kenyatta wa Jubilee ana kura 7,461,933 (54.64%) Raila Odinga wa ODM kura 6,079,136 (44.51%) Joseph Nyagah (huru) 33,710 (0.25%) Abduba Dida wa ARK 29,411 (0.22%) Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance 23,976 (0.18%) Japheth Kaluyu (huru) 10,316 (0.08%) Cyrus Jirongo wa UDP 10,019 (0.07%) Michael Wainaina (huru) 7,919 (0.06%) Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 353,389 Ili kushinda, mgombea urais anahitajika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na angalau asilimia 25 katika kaunti 24 kati ya kaunti 47 nchini humo. Iwapo hakuna mgombea atakayetimiza hilo, basi uchaguzi wa marudio utafanyika katika kipindi cha siku 30.

Popular posts from this blog

LIST OF THE OLDEST UNIVERSITY IN AFRICA

LIST YA MIJI HATARI NCHINI MAREKANI

Top 7 Questions and Answers on Leadership